1. Leibniz-Zentrum Moderner Orient
  2. Events
  3. Detrimental Effects of Chinese Infrastructure Projects on the Lives of Kenyan and Tanzanian Residents
Events
Lecture, Lecture series

Detrimental Effects of Chinese Infrastructure Projects on the Lives of Kenyan and Tanzanian Residents

Swahili Baraza with Aldin Mutembei (University of Dar es Salaam), Daniel Koßmann (HU Berlin) and Kadara Swaleh (ZMO)

Ndugu waheshimiwa, wapendwa wanafunzi na marafiki zetu,

Baada ya kikao maalum chenye konsati ni furaha yetu kutangaza kikao kifuatacho cha Baraza letu la Kiswahili la Berlin (BALAKI-BE) la tarehe 26 Juni 2023: Madhara ya Miradi ya Miundombinu ya Uchina kwa Maisha ya Wakazi wa Kenya na Tanzania

Aldin Mutembei, Daniel Koßmann na Kadara Swaleh

Katika kikao hiki tutakuwa na mjadala wa jopo unaowajumuisha wataalamu wa mradi wa utafiti wa De:link/Re:link unaofadhiliwa na Wizara ya Elimu na Utafiti ya Ujerumani na kuangazia mbinu mpya na mitazamo ya ndani ya kufahamu miradi ya miundombinu ya Uchina huko Afrika Mashariki na kwingineko katika muktadha wa Miradi ya Ukanda na Barabara (BRI).

Kadara Swaleh ni mtafiti wa Taasisi ya Mashariki ya Kisasa (ZMO) huku Berlin na mwanafunzi wa uzamili wa Chuo Kikuu Huru cha Berlin. Ataangazia athari za mradi wa miundombinu ya Uchina (SGR) kwa wakazi wa Mombasa kwa kuzungumzia maendeleo ya utafiti wake aliowahi kutambulisha barazani kwetu.

Daniel Koßmann naye anasomea shahada ya tatu akiwa ni mtafiti wa Taasisi ya Taaluma za Afrika na Asia ya Chuo Kikuu cha Humboldt Berlin. Atayajadili masuala ya mtafiti mwenzake kwa kurejelea pia uchambuzi wake wa mienendo mipya katika eneo la kitamaduni na kisanii jijini Dar es Salaam tangu taasisi ya Confucius ilipofunguliwa mwakani 2013.

Profesa Aldin Mutembei ni Mgoda, Kigoda cha Kiswahili cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius ya chuo hicho. Atayatolea hoja na nasaha tafiti za waliotajwa hapo juu akirejelea pia ufundishaji wa Kichina na lugha nyingine za kigeni katika muktadha wa kukuza lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kiafrika.

Kikao kitafanyika siku ya Jumatatu, tarehe 26 Juni 2023, saa kumi kamili za Ulaya ya Kati (saa kumi na moja za Afrika Mashariki) Zentrum Moderner Orient, Kirchweg 33, 14129 Berlin. Pia kitapatikana kupitia njia ya Zoom kama kawaida:

https://us02web.zoom.us/j/87403517259?pwd=SDZNSmNoS3AybitaL3N4VWNPWEEzUT09

KARIBUNI NYOTE!

Tafadhalini wajulisheni wapenzi wote wa Kiswahili na marafiki wengine!

Wasalaam,
Kai Kresse, Lutz Diegner na Maxwell Omondi Ondieki

Kama kuna maswali yoyote kuhusu baraza hili tafadhalini mwandikieni mwenzetu: MaxwellOmondi.Ondieki(at)zmo.de

This event is part of the lecture series:
Presentation and Discussion Sessions in Swahili 2023
Baraza la Kiswahili la Berlin

Details