1. Leibniz-Zentrum Moderner Orient
  2. Events
  3. Masuala ya Kiuana katika Vitabu vya Fasihi Vilivyoteuliwa na Wizara ya Elimu ya Kenya
Events
Lecture, Lecture series

Masuala ya Kiuana katika Vitabu vya Fasihi Vilivyoteuliwa na Wizara ya Elimu ya Kenya

Catherine Ndungo (Chuo Kikuu cha Kenyatta)

Katika wasilisho hili Profesa Ndungo atayajadili masuala ya kiuanakatika vitabu vilivyoteuliwa na Wizara ya Elimu ya Kenya kusomwa katika somo la fasihi ya Kiswahili katika shule za upili kwa kuzingatia nadharia ya ABC ya uchambuzi wa kiuana (1997). Waasisi wa nadharia hiyo ni Profesa Wanjiku Kabira (Idara ya Fasihi, Chuo Kikuu cha Nairobi) na Dk Masheti Masinjila (Katibu Mtendaji wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Collaborative Centre for Gender and Development). Mada hii ni muhimu tukizingatia kwamba nadharia hii ndiyo inatumiwa na Taasisi ya Elimu ya Kenya kama mwongozo wa kutathmini ufaafu wa vitabu vya fasihi katika misingi ya kiuana. Masuala ambayo yatajadiliwa ni maudhui, usawiri wa wahusika na matumizi ya lugha katika vitabu ambavyo vinasomwa sasa na wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne katika shule za sekondari. Vitabu hivi ni tamthilia ya Kigogoambayo imeandikwa na Pauline Kea (2016), riwaya ya Chozi la Heriambayo imeandikwa na Assumpta Matei (2017) na mkusanyiko wa hadithi fupi wa Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingineuliohaririwa na Alifa Chokocho na Dumu Kayanda (2016). Msimamo wetu ni kwamba uteuzi wa vitabu hivi haukuzingatia kero za kiuana ambazo zinaikumba jamii ya kisasa.

Catherine Ndungoni Profesa Mshirikishi katika Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi, Kenya. Ana Shahada ya Uzamivu ya chuo hichohicho, na Shahada ya Uzamili na Ukapera kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Amefundisha zaidi ya miaka thelathini katika Idara ya Kiswahili. Ni mwanzilishi wa Idara ya Uana na Maendeleo na mwenyekiti wa kwanza wa idara hiyo. Baadaye alianzisha Taasisi ya Masomo ya Kiafrika na kuwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo. Amechapisha vitabu ambavyo vimeiidhinishwa na Taasisi ya Elimu ya Kenya kama vitabu vya kutumiwa na wanafunzi katika shule za msingi na za upili. Vilevile ni mtunzi wa hadithi fupi. Ameandika makala mengi juu ya masuala ya lugha, fasihi, uana na uongozi. Sasa hivi anatafiti juu ya mikakati na sera za kuwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kushiriki katika masuala ya kiuchumi, mradi ambao unadhaminiwa na Melinda Gates Foundation.

Mkiwa na maswali karibuni mtuandikie baruapepe: Augustine.Malija@zmo.de

This event is part of the lecture series:
Presentation and Discussion Sessions in Swahili
Baraza la Kiswahili la Berlin

Details