1. Leibniz-Zentrum Moderner Orient
  2. Events
  3. One Day at the Office: Upapasi, Spatial Il/legalization and Matter in Urban Zanzibar
Events

One Day at the Office: Upapasi, Spatial Il/legalization and Matter in Urban Zanzibar

Swahili Baraza with Muchi and Irene

Ndugu waheshimiwa, wapendwa wanafunzi na marafiki zetu,

Baada ya mwezi wa mapumziko ni furaha yetu kubwa kutangaza kikao kifuatacho cha Baraza letu la Kiswahili la Berlin (BALAKI - BE) ambacho kitakuwa na mada ifuatayo: 
Siku moja ofisini: upapasi, uwenyeji/ na u/ki/tu mjini Zanzibar

Katika mazungumzo na majadiliano baina ya Muchi na Irene, wasilishaji hao wawili wanatuhadithia kuhusu kikundi cha vijana wanaoitwa mapapasi ambao wanafanyia kazi Sekta ya Utalii mjini Zanzibar tangu miaka ya Themanini, ijapokuwa mchango wao katika uchumi haujatambuliwa au kurasimishiwa na Serikali. Badala yake, mara nyingi vijana hao wanaudhiwa, wakipuuzwa na kuadhibishwa kwa vile hawapaswi kwenye picha ya kiserikali ya kukuza Zanzibar kama mahali pa misafara ya Watalii. Muchi na Irene wanalinganisha kazi ya Upapasi vile ilivyokuwa zamani na vile ilivyo sasa hivi. Pia, wanatafakari kuhusu nafasi ya mapapasi mjini Zanzibar na katika hi/storia ya kijamii na kiuchumi visiwani huku wakichambua dhana ya uwenye/ji, maana, athari na umuhimu wake. Mwishowe, wanajadiliana na Wanabaraza kuhusu uwezo wa dhana ya u/ki/tu, pale wanapojitahidi kuelewa na kutafsiri nafasi ya watu, vitu, maneno na vitendo kwenye kutafuta na kujenga maisha.

Muchi ni papasi anayefanya kazi mjini Zanzibar, kisiwani Unguja. Amekuwa maarufu sana kwa sababu ya kazi na roho yake safi. Anajulikana sana Zanzibar na Ugenini kwa kuwa gwiji miongoni mwa Mapapasi tangu miaka kadhaa.
Irene ni Mwalimu wa lugha katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Leipzig. Amefanya utafiti mbalimbali na kuandika kuhusu ngoma za KiZanzibari, CyberBaraza, Ushairi, Taaluma za mjini, na Uswahili kwa jumla. Kwa sasa, anafanya utafiti kuhusu uhusiano baina ya maneno, vitu, vitendo na watu kwenye kujeng(u)a dhana mbalimbali.

Kikao kitafanyika siku ya Jumatatu, tarehe 13 Juni 2022, saa kumi kamili za Ulaya ya Kati (saa kumi na moja za Afrika Mashariki) kupitia njia ya Zoom: https://tinyurl.com/5c9m7hjr

KARIBUNI NYOTE! 

Tafadhalini wajulisheni wapenzi wote wa Kiswahili na marafiki wengine!

Wasalaam,
Kai Kresse, Lutz Diegner na Maxwell Omondi Ondieki

Kama kuna maswali yoyote kuhusu baraza hili tafadhalini mwandikieni mwenzetu: MaxwellOmondi.Ondieki(at)zmo.de
 

This event is part of the lecture series:
Presentation and Discussion Sessions in Swahili 2022
Baraza la Kiswahili la Berlin

Details