Baraza letu la Kiswahili la Berlin (BALAKI‐BE)
Baraza letu la Kiswahili la Berlin (BALAKI‐BE) la tarehe 10 Januari 2022
Aibu, Dini na Mazao: Urithi wa Utumwa katika Bara la Afrika Mashariki
Felicitas Becker
Inaonekana kwamba utumwa umefutika kwa urahisi huko bara la Afrika Mashariki, tofauti na sehemu nyingi kwingine. Matokeo hayo ni mafanikio ya aina yake kwa jamii za bara, yaani zimeepukana na mizozo mingi inayohusiana na historia ya utumwa katika maeneo mengine. Hata hivyo, ni vigumu kuulizia habari za utumwa huko bara. Hali hii inaonesha kwamba mambo hayo bado yana nguvu fulani ya kugawanya watu. Kwa kuzingatia hayo, uwasilishaji huu una malengo mawili. Kwanza, unachunguza namna utumwa kama njia ya kutoza nguvukazi ya watu ulivyotoweka wakati wa ukoloni. Katika mchakato huu, mabadiliko ya kiuchumi na ya kidini yote mawili yalikuwa muhimu. Pili, unachunguza maana ya ‘aibu’ inayozuia watu wasiongelee utumwa, yaani namna utumwa uliendelea kuwepo kama chimbuko la tofauti za hadhi katika jamii. Je ni nani hasa anayetarajiwa aone aibu? Na sababu za kuona aibu ni zipi hasa? Lengo la uwasilishaji huu ni kuelewa namna ambavyo utumwa umebaki mwiko, hata kama watu husisitiza kwamba umetoweka kabisa.
Felicitas Becker ni Profesa wa Historia ya Afrika huko Chuo Kikuu cha Ghent, Ubelgiji. Amesoma huko Berlin, London na Cambridge, na amesomesha huko Budapest, London, Vancouver na Cambridge. Utafiti wake huushughulikia Uislamu, hasa vijijini, umaskini na maendeleo vijijini, harakati za wahubiri wa Kiislamu na athari za utumwa, hasa maeneo ya Tanzania Bara.
Kikao kitafanyika saa kumi kamili za huku Berlin ( saa kumi na mbili kamili za Afrika Mashariki) hadi saa kumi na mbili kasoro (saa mbili kasoro za Afrika Mashariki) kwa njia ya Zoom: https://us02web.zoom.us/j/88599256889?pwd=SzBHd0FTb2s0WS9aYURhUVlsWVhqUT09
KARIBUNI SANA!
Tafadhalini wajulisheni wapenzi wote wa Kiswahili na wenzenu wengine!
Wasalaam,
Kai Kresse, Luti Diegner & Maxwell Omondi
Kama kuna maswali yoyote kuhusu baraza hili tafadhalini mwandikieni mwenzetu: maxwellomondi@zmo.de
Diese Veranstaltung gehört zur Vortragsreihe
Swahilisprachige Veranstaltungsreihe
Baraza la Kiswahili la Berlin
Veranstaltungsdetails
Online